- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Rais Samia Suluhu Hassan amesema tuzo aliyotunukiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe, imempa nguvu na motisha zaidi ya kuandaa kwa ufanisi Mashindano makubwa ya soka kwa Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, yatakayoandaliwa kwa pamoja na Kenya na Uganda.
Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha mchana aliyoiandaa kwa ajili ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) pamoja na wanamichezo wengine waliofanya vizuri katika michezo mbalimbali, Rais Samia amesema tuzo hiyo ni heshima kubwa na imempa hamasa ya kuhakikisha maandalizi ya michuano hiyo yanafanyika kwa kiwango cha juu.
Ameongeza kuwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kukuza mchezo wa soka nchini ni chachu kwa Tanzania kufanya vizuri zaidi siyo tu katika soka, bali pia katika michezo mingine.
Ikumbukwe pia kuwa Novemba 19, 2025, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) lilimtunuku Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Uganda Yoweri Museveni tuzo ya heshima kwa mchango wao katika kuandaa kwa mafanikio michuano ya CHAN.
RAIS DKT. SAMIA: WALIOTAKA KUVURUGA AMANI NA KUCHAFUA SIFA YA TAIFA LETU WASHINDWE NA WALEGEE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema amepokea tuzo tatu za kimataifa akiwa Zanzibar, ikiwa ni matokeo ya juhudi za serikali katika kulinda amani, kuimarisha utalii na kutangaza taswira chanya ya nchi.
Rais Samia amesema Tanzania imepewa kikombe cha kutambuliwa kama nchi bora ya utalii barani Afrika, pamoja na tuzo ya kuwa miongoni mwa nchi bora za utalii duniani. Aidha, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pia imepewa tuzo maalumu kutokana na mchango wake mkubwa katika uhifadhi na kuvutia watalii duniani.
Vilevile, Zanzibar imepokea tuzo ya kutambuliwa kama mji bora wa mikutano ya kimataifa, hatua inayothibitisha hadhi yake katika sekta ya utalii wa mikutano na uwekezaji.
Akizungumzia mafanikio hayo, Rais Samia amesisitiza kuwa tuzo hizo ni ushahidi wa amani, mshikamano na sifa njema ya Tanzania kimataifa. Ameongeza kuwa jitihada zozote za kuharibu amani na taswira ya taifa hazitafanikiwa, akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani.
“Kwa waliotaka kutuharibia amani na kuichafua sifa ya taifa letu, washindwe na walegee. Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani,” amesema Rais Samia.
RAIS DKT. SAMIA: DUNIA IMEONA WAZI TULIPAMBANA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewapongeza wachezaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa kufanikiwa kufika hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON, akieleza kuwa ni mafanikio makubwa kwa taifa.
Akizungumza leo Ikulu wakati wa chakula cha mchana alichokiandaa kwa ajili ya kuzungumza na timu hiyo, Rais Samia pia aliizungumzia mechi kati ya Morocco na Tanzania, akibainisha kuwa mchezo huo ulikuwa na utata wa hapa na pale.
Rais amesema kuwa Tanzania ilicheza dhidi ya timu mwenyeji na yenye ushawishi mkubwa, akisisitiza kuwa kilichotokea kinaeleweka kutokana na mazingira ya mashindano. Hata hivyo, ameeleza kuwa juhudi na mapambano ya wachezaji wa Taifa Stars yalionekana wazi, si kwa Watanzania pekee bali pia kwa dunia nzima.
“Tulicheza dhidi ya wenyeji, taifa lenye fedha na ushawishi mkubwa kwa waandaaji, lakini tuliona wazi, na dunia imeona wazi, kwamba Tanzania ni wapambanaji na wamepambana,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono wachezaji na sekta ya michezo kwa ujumla, akiwahimiza Taifa Stars kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuiletea nchi heshima katika mashindano yajayo.
RAIS DKT. SAMIA AKABIDHIWA TUZO KUTOKA CAF
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo amepokea tuzo ya jezi maalumu kutoka kwa wachezaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), jezi iliyosainiwa na baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho, kama ishara ya heshima na shukrani kwa mchango wake katika maendeleo ya michezo nchini.
Hafla hiyo imefanyika leo Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa chakula cha mchana, ambapo Rais Samia amekutana na wachezaji, viongozi wa michezo pamoja na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Aidha, Rais Samia pia amepokea tuzo nyingine kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ikiwa ni kutambua ushiriki wake na kuunga mkono jitihada za maendeleo ya michezo, hususan mpira wa miguu, ndani na nje ya nchi.
Katika hafla hiyo, viongozi wa michezo wamepongeza uongozi wa Rais Samia kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya michezo, kuimarisha michezo ya vijana, na kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika mashindano ya kimataifa.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Rais Samia ameahidi kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya michezo ili kuibua vipaji, kuongeza ajira kwa vijana na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia michezo.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa