- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Kaimu Mkurugenzi wa wilaya ya Ngara Gideon Mwesiga amewahasa wanasemina kuwaelimisha wananchi katani Kibogora kuhusu athari za mabomu ili waweze kuwatuliza kisaikolojia. Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kujikubali na hivo kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya msaada wa kisaikolojia kwa wahanga wa mlipuko wa bomu katika shule ya msingi Kihinga mwishoni mwa mwaka jana. Mafunzo hayo yanafanyika katika shule ya sekondari ya Kibogora katika kata ya Kibogora.
Mafunzo hayo yatakayodumu kwa siku tano yanaratibiwa na shirika la Jambo Bukoba. Mafunzo yanawajumuisha Diwani wa kata ya Kibogora Mh. Adroniz E. Burindoli, wazazi, wakuu wa shule za msingi, maafisa Elimu Kata wa kata za Bukiriro na Kibogora, watoto 30 kutoka katika shule za msingi Kihinga, Nyarukubala na Nyarulama pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Kibogora.
Katika mafunzo hayo mada zinazofundishwa ni ullinzi na usalama kwa watoto, malezi na msaada wa kisaikolojia, mafunzo juu ya hisia, uwezo wa kurejea katika hali ya kawaida na namna ya kujikinga na mabomu.
Amesema mafunzo hayo yatakuwa na maana na kutimiza lengo lake ikiwa waliohudhuria watawashirikisha wananchi wenzao ambao hawakupata mafunzo hayo kile walichojifunza, vinginevyo yatakuwa hayana maana.
Akisistiza alisema kuwa, kama watawashirikisha wenzao watakuwa wamewasha taa iwamulikie wote, kinyume chake watakuwa wamewasha taa na kuiweka chini ya uvungu wa kitanda.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuwashukuru baadhi ya wadau waliotoa misaada ya hali na mali kuhakikisha kuwa waathirika wanapata matibabu na mafunzo ya kisaikolojia, kuwa ni Jambo Bukoba, Chama cha Walimu, Tumain Fund, Caritas, wafanyabiashara, na wanajeshi wa jeshi la wananchi wa Tanzania.
Alisema kuwa Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni tisa kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu za wahanga wa bomu waliotibiwa katika hopitali ya Kagondo na wale watakaokwenda kutibiwa KMC Moshi.
Naye Meneja wa Jambo Bukoba Ndg. Gonzaga Stephan amesisitiza kuwa wanaweza kufanya kazi katika mazingira salama kama hakuna hofu ya ulipukaji wa mabomu. Aidha ameongeza kuwa mtoto anapoathirika hata Jambo Bukoba inaathirika, ndiyo maana wanaratibu mafunzo haya ili kunyumbulisha maisha ya watoto ili warejee katika hali yao ya kawaida.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa