- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Waumini wa madhehebu yote hapa nchini, wametakiwa kuishi kadiri ya utaratibu na malengo ya Mwenyezi Mungu, unaowataka mume na mke kusaidiana, kuzaa pamoja na kuitawala dunia, huku wakiwalea watoto wao, katika maadili yanakubalika kidini na kijamii.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara Mhashamu Sevelin Niwemugizi, ameyasema hayo ofisini kwake Mei 17, 2019; kwamba wanafamilia wamemweka Mwenyezi Mungu pembeni, matokeo yake jamii inakata tama na kukosa mwelekeo.
Baba Askofu Niwemugizi anaamini kwamba suala la familia kuwa na imani na maadili yaliyotukuka, haliwahusu waumini wa dhehebu fulani tu, bali ni suala la kijamii zaidi; akidai kwamba kama jamii ipo, ni kwa sababu kuna ndoa na vitu vya msingi vinavyoigusa.
“Ikishafikia mahali wanafamilia wakamweka Mwenyezi Mungu pembeni, wakamuweka nje ya mipango/utaratibu wa maisha yao, ndiyo mwisho wa familia hiyo. lazima wanafamilia wamshukuru na kumwomba Mungu awabariki.” Amesema Askofu Niwemugizi.
Baba Askofu anasema lengo la kwanza la wanandoa ni kusaidiana kama Maandiko Matakatifu yanavyosema, mume na mke wasaidiane, wazae na waongezeke; lakini Mwenyezi Mungu akawapa kazi nyingine ya kuitawala dunia. “Sasa tujiuliza katika jamii ya leo haya malengo watu wanayaishi?”
Kinyume na malengo ya Mwenyezi Mungu Baba Askofu Niwemugizi, anasema kwamba watu wanaoana kwa malengo tofauti; mwingine anataka mtu wa kumzalia mtoto tu, mwingine anataka mali na mwingine anataka msomi, na kuongeza kwamba ndoa ni zaidi ya hayo, ndiyo maana jamii imetunga sheria ya ndoa.
Katika kuzaa kuna wajibu wa kulea, ambayo ni pamoja na kuelimisha, kutia maadili mema, nidhamu na kuwaelekeza watoto katika imani, wazazi kama walivyofunuliwa na Mwenyezi Mungu, imewapasa kuwavuvia maadili mema watoto wao, ili wawe raia wema, na waumini wanaoishi kadiri ya maelekezo ya Mwenyezi Mungu.
“Lakini nasikitika kwamba mambo hayako hivyo; watu wanaingia kwenye ndoa kwa malengo yao au kwa miunganiko ya ajabu tunayoisikia; mimi nasema, tukitaka kwenda sawa; lazima jamii irudi nyuma iangalie mpango wa Mwenyezi Mungu kwetu sisi ni upi? Je huu mpango tunauheshimu na kuishi?” Aliuliza Askofu Niwemugizi.
Amesema mtu anaamuka asubuhi anaondoka kwenda kutafuta fedha, lakini anasahau kumtanguliza Mwenyezi Mungu, anayemwezesha kutafuta fedha/mali, hivyo akawashauri wamtangulize Mwenyezi Mungu, ili awabariki kwa kuwapatia watoto waadilifu na mali.
Aidha, amewataka wanafamilia kuwa na utulivu wa ndani; akimaanisha kila mwanafamilia, apate muda wa kutafakari na kujitazama; ametoka wapi, yuko wapi na anakwenda wapi; na kudai kwamba hiyo ni sifa muhimu kwa wanafamilia.
Amewahimiza wanafamilia wanapokabiliana na changamoto wajiweke mbele ya Mwenyezi Mungu na kumwambia tatizo lao, ili aweze kuwaonyesha njia ya kuyashinda yanayowakwaza na kuwapeleka kusikofaa.
Tabia mbaya zinazoonekana katika jamii zetu, chanzo chake ni familia; akitoa mfano ametaja mihemko, unyanyasaji, wivu, mauaji, ukatili, ubakaji/ulawiti na hata ushirikina vinaanzia kwenye familia; ambavyo amevitaja kuwa ni matokeo ya familia zisizomtanguliza Mwenyezi Mungu.
“Kama ni nidhamu tunayoiona sehemu zetu za kazi, shuleni na kwingineko, vinaanzia kwenye familia, ndiyo maana tukitaka kurekebisha mambo, kuwa na utulivu na amani, lazima tuanzie kwenye familia.” Alisema Baba Askofu Niwemugizi.
Kufuatia jamii kubadilika; Baraza la Maaskofu Katoliki la Tanzania, limeamua kuwaongoza waamini wake, kuwambudu Mwenyezi Mungu kuanzia ngazi ya familia, kwenye jumuia ndogo ndogo na kisha kwenye Ibada ya Misa takatifu kila Jumapili.
“Sisi Maaskofu Katoliki Tanzania, tuliwaomba waumini wetu wakati wa Kwaresima, watafakali juu ya familia kama kanisa la nyumbani, na shule ya imani na maadili; wakitumaini kwamba waamini wakirithishana imani yao, na wakajikabidhi kwa Mungu; watakuwa imara, na familia zao zitabaki salama.” Alisema Mhashamu Niwemugizi.
Mwenyezi Mungu, aliwaumba mke na mume, ili wazae na waongezeke, na kwa mpango huo, tunapata tunda la ndoa ambalo ni familia, inayowajumuisha Baba na Mama na baadae watoto; ambapo maandiko matakatifu yanasema “tumeumba vitu vyote, lakini hatujaumba kitu kinachofanana nasi.”
“Mungu anasema tufanye mtu kwa mfano wetu na sura yetu, alipomuumba Adamu akalifika mahali akasema, lakini huyu mtu ataishije peke yake!! Lazima huyu awe na msaidizi wake, akamtengeneza mwanamke akasema, huyo atakuwa msaidizi wake.” Alisema Askofu Niwemugizi.
Aidha, kadiri ya Baba Askofu huyo, ndoa ni muungano kati ya mume na mke, lakini kunyume na hekima na Busara ya Mwenyezi Mungu; changamoto mbalimbali katika jamii zinasababisha waumini wakiuke makusudi ya Mwenyezi Mungu, ambapo leo hii Mwanaume na Mwanaume wanaoana.
Katika jamii yetu imepita Sunami (Utandawazi) na kuwaacha wanafamilia, wakishangaa na kulalamikia kuvunjika kwa maadili, Baba Askofu anaiona familia kama mti wa matumaini, ambao lazima ulishwe mbolea, ili baadae utoe mbegu zilizo njema.
Aidha, mmonyoko wa maadili katika jamii, umepelekea Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kutafuta mbinu mbadala ya kuwafunda vijana, wanaotaka kumtumikia mwenyezi Mungu kama mapadre, ili waweze kuitambua jamii walimotoka na wawe tayari kuisaidia wakishapadrishwa.
“Sisi hatutoki kwenye kisiwa, tunatoka kwenye familia zetu, zilizokwishaathirika na yanayoendelea, kwa mfano, kutojali imani, na baadhi ya wazazi hawasali kabisa; hilo tumeliona na tunajua kwamba ni changamoto kubwa sana.” Alisema Baba askofu Niwemugizi.
Amesema tofauti na zamani vijana wengi, walipokuwa wakifundshwa maadili mema wakiwa seminari ndogo, siku hizi wanapata changamoto ya kupata vijana wengi kutoka shule za kata, kwa hiyo, wanahitaji kufanyakazi ya ziada, kuwaandaa vijana hao, kwa ajili ya kazi hiyo muhimu.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa