- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Mh. Vedastus Edger Ngombalemwiru ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, kuacha tabia ya kubadili usanifu wa miradi bila kufuata ushauri na taratibu zilizopo.
Mh. Ngombalemwiru amesema haya wakati wa majumuisho baada ya kamati hiyo, kutemebelea miradi ya Maji ya Munjebwe na Mbuba Machi 26, 2019, iliyoanza kujengwa mwaka 2013 hadi 2019 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 813.
“Baada ya kukagua miradi ya maji ya Munjebwe na Mbuba, tumabaini kwamba kulikuwa na udhaifu katika kutekeleza miradi hii, hali iliyopelekea mradi wa Munjebwe kujengwa chini ya kiwango.” Alisema Mh. Ngombalemwiru.
Kadiri ya Mwenyekiti huyo, kulikuwa na marekebisho yaliyofanywa katika mikataba bila kufuata taratibu zilizopo, na kuiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kuwakilisha nyaraka za mabadiliko hayo kwa CAG, ifikapo Juni 01, 2019 kwa ajili ya kuyafanyia uhakiki.
Wameiagiza Halmashauri hiyo, kuhakikisha mapungu yote ya mradi wa maji wa Munjebwe, yamerekebishwa kwa kutumia ‘detention money’ kama Mhandisi na Mkurugenzi, walivyoahidi na taarifa ya utekelezaji huo, iwasilishwe kwa CAG na kamati hiyo kabla ya tarehe 01/06/2019.
Aidha, wameagiza mwanasheria wa RAS, ashirikiane na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, kuhakikisha kwamba doasari za kisheria zilizojitokeza zinarekebishwa na makubaliano ya sasa yanakuwepo kisheria; ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza baadae.
Pia, wameitaka ofisi ya Mkuu wa Mkoa na TAMISEMI, kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, inapata mwanasheria, atakayetoa ushauri wa kitaalamu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.
Kadiri ya Mhadisi wa Idara ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Eng. Simon Ndyamukama, mradi wa maji wa Munjebwe ulianza kutekelezwa mwaka 2013 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 287.
Akijibu maswali ya wanakamati, Eng. Ndyamukama amekiri kwamba mradi huo haujawanufaisha wananchi kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika mradi huo, ikiwemo kuvuja kwa tenki na kupelekea baadhi ya wananchi walengwa wa mradi huo kutopata maji kama ilivyokusudiwa.
Eng. Ndyamukama ameiambia kamati kwamba kutokana na mapungufu hayo, mradi bado uko mikononi mwa mkandarasi hadi marekebisho hayo yatakapo fanyiwa kazi, na wananchi wakapata huduma ya maji kadili ya makusudi ya serikali.
Wananchi wa Kijiji cha Munjebwe wamethibitisha kuwa maji wanayopata kutokana na mradi huo, yanakuwa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi ya wananchi hao.
Akisoma taarifa ya mradi wa maji wa Mbuba, Eng. Ndyamukama, amesema kwamba mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2014 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 524, lakini hadi sasa haujakamilika kwa sababu ya serikali kuchelewesha fedha ya kulipa madai ya mkandarasi.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Ndugu Erick Nkilamachumu, ameiomba Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, kuishauri serikali kuleta fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati, ili miradi hiyo ikamilishwe kwa wakati.
“Kwa sababu ninyi mko Bungeni naomba muishauri serikali, watuletee fedha kwa wakati kwa ajili ya miradi inayotekelezwa huku vijijini; kwa sababu haingii akilini kwamba miradi ya maji ya mwaka 2013 hadi 2019 bado haijakamilika.” Alisema Ndugu Nkilamachumu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Ndugu Aidan John Bahama, ameiambia kamati hiyo, kwamba watahakikisha ushauri uliotolewa na kamati hiyo, unafanyiwa kazi, ili miradi iwe na tija kwa wananchi.
Ndugu Bahama ameishukuru kamati hiyo kwa kuichagua Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, kwani mapendekezo yanayotolewa, yanalenga kuleta ufanisi wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya mlengwa, ambaye mwananchi.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa