- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Mkuu wa mkoani wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, ameagiza wakala wa misitu TFS kuruhusu halmashauri nane za wilaya mkoani humo, kukata miti ya kutengeneza viti na meza, kwa ajili ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2019.
Brig. Jen. Gaguti ametoa agizo hilo Desemba 20, 2018, wakati akishiriki kipindi cha Asubuhi njema kinachotangazwa na Radio Kwizera wilayani Ngara, akielezea mkakati wa kujenga vyumba 315 vya madarasa ambavyo inabidi vikamilike ndani ya miezi mitatu ijayo.
“Kutokana na changamoto ya kukosa vyumba vya madarasa, Halmashauri nimeelekeza, kutumia vyumba vya maabara, ambavyo havina vifaa vya masomo ya sayansi kwa kipindi cha miezi mitatu, kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi 14,046, waliofaulu na kukosa madarasa.” Alisema Brig. Jen. Gaguti.
Alisema wakala wa misitu TFS wakitoa miti, kila halmashauri itatumia mafundi wake kutengeneza samani hizo, kwa kutumia baadhi ya fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali katika sekta ya elimu badala ya mzigo huo kuwaachia wazazi na walezi pekee.
"Mkakati wa mkoa ni kushirikisha wadau kama taasisi za kibenki na wadau wote wa elimu wenye nia njema ya kuunga juhudi za serikali kwa kutoa fedha za kujenga vyumba vipya vya madarasa,pamoja nakufanya mikutano ya harambee kwa lengo la kuondoa changamoto hiyo" Alisema Brig. Jen. Gaguti.
Pamoja na mkakati wa kutumia vyumba vya maabara, bado mkoa huo unahitaji zaidi vyumba 352 vya maabara kutosheleza mahitaji ya maabara 570, ambapo baadhi yake vilibadilishwa kutoka madarasa ya kawaida, na kuwekewa miundombinu kwa ajili masomo ya sayansi.
Baadhi ya wananchi wamemtaka mkuu huyo wa mkoa kuruhusu hata hayo majina ya wanafunzi waliofaulu, lakini hawakupata nafasi za vyumba vya madarasa kutangazwa, ili watafutiwe mahitaji ya sare na vifaa vya kujifunzia.
Mmoja wa wananchi waliopiga simu kuchangia mjadala wa kipindi cha Asubuhi njema aliyejitambulisha kwa jina la Stela Thimotheo kutokea Biharamulo; alisema wazazi wamebaki bila kujua watoto waliofaulu watakwenda shule zipi, wakati muda wa kuanza masomo Januari umekaribia.
Naye Oscar Silvester kutoka kata ya Kyebitembe wilayani Muleba, alishauri serikali ikiweka mipango na mikakati ya ujenzi wa miradi ya maendeleo, viongozi wa wilaya na wa mkoa wafike kwenye eneo husika, ili kujiridhisha na utekelezaji huku wakibaini changamoto zinazowakabili wananchi na kuzirekebisha.
Wiki iliyopita waziri wa TAMISEMI Suleiman Jaffo, alisema mikoa ya Kagera na Kigoma imefaulisha wanafunzi wengi, lakini wamekosa vyumba vya madarasa, ambapo mkoa wa Kagera unao jumla ya wanafunzi 14,046 na Kigoma wanafunzi 12,178.
Watahiniwa waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2019 mkoani wa Kagera ni watoto 39,545, ambapo wavulana ni 18, 553 na wasichana ni 20,992, huku kiwango cha ufaulu mwaka 2018 kikipanda kwa asilimia 0.02% pekee.
Mwaka 2018 mkoa wa Kagera ulikuwa na watahiniwa 47,197, waliotarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, kati yao wavulana walikuwa 22,124, na wasichana ni 25,073, ambapo watahiniwa 86 walikuwa wenye mahitaji maalumu; wavulana ni 50, na wasichana 36.
Mchanganuo wa wanafunzi waliofaulu, lakini hawakupata nafasi kuoka kila Halmashauri mkoani Kagera ni kama ifuatavyo; wanafunzi 2160 kutoka Biharamulo, Bukoba DC 877, Bukoba Manispaa 1276, Karagwe 3086, Kyerwa 1876, Missenyi 578, Muleba 3696 na wanafunzi 256 kutoka Ngara.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa