- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Kamati ya lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, imetakiwa kuhakikisha inatekeleza shughuli za kutokomeza udumavu wa watoto, kama ilivyoainishwa katika mkataba wa mradi wa Mtoto Mwerevu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Ndugu Gideon Samson Mwesiga, ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya lishe, kilichofanyika Oktoba 10. 2018 katika ukumbi wa Halmashauri.
“Kamati ya lishe ya wilaya ihakikishe inasimamia na kutekeleza majukumu yake ya kupunguza udumavu kila mjumbe kutambua majukumu yake hasa kuielimisha jamii itambue athari za udumavu na jinsi ya kuutokomeza.” Alisema Mwesiga.
Amewataka wajumbe wa kikao hicho kujadili shughuli za lishe, zilizofanyika katika kipindi cha Julai - Septemba 2018, ili kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi katika suala zima la lishe bora kwa watoto.
Wakati huo huo, Mratibu wa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Ndugu John Sosthenes amesema kupitia Mradi wa Mtoto Mwerevu kwa kutumia watoa huduma ngazi ya jamii (WAJA) wajawazito na watoto chini ya miaka miwili wamepata elimu ya kubadili tabia ya masuala ya lishe bora.
Amesema tabia hizo zimegawanyika katika makundi tofauti ambapo ya kwanza inajumuisha umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi 6, bila mtoto kupewa chakula chochote hata maji.
Amesema kwamba baada ya miezi 6 mtoto apewe chakula cha nyongeza chenye virutubishi vyote muhimu; huku akiitaja tabia ya tatu kuwa ni usafi wa mazingira, na tabia ya nne ni ushiriki wa akina baba katika malezi na makuzi ya mtoto.
Alisisitiza kwamba katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2018, licha ya kuwa na changamoto ya kutopata fedha kwa wakati, wamefanikiwa kufanya usimamizi elekezi kwa WAJA, juu ya utoaji elimu sahihi kwa walengwa wa mradi wa mtoto mwerevu.
Aidha, wamefanikiwa kutoa matone ya vitamin A kwa watoto wa miezi 6-59, utoaji wa madini chuma kwa wakina mama wajawazito, unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa watoto (EBF) na akina mama wenye watoto miezi 0-23.
Kikao hicho kiliwasilisha shughuli za utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha julai hadi septemba 2018, na kujadili taarifa za utekelezaji wa shuguhuli za lishe katika kipindi cha miezi mitatu, na kutambulisha shughuli ya kutokomeza utapiamlo (Positive Deviance Hearth).
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa