- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Wahamasishaji na watoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za ugonjwa wa Ebola katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, wametakiwa kwenda kutoa elimu hiyo vijijini kwani wananchi hao bado hawana uelewa wa ugonjwa huu, ikilinganishwa na wale wa mjini.
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, ambaye ni mwenyekiti wa kikao cha kikosikazi cha Kupambana na Ugonjwa wa Ebola wilayani Ngara Lt. Col. Michael Mntenjele, ametoa wito huo wakati wa kikao cha kuweka mikakati ya jinsi ya kudhibiti ugonjwa huo wilayani humo.
Kikaokazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu waWilaya Januari 09, 2019; kiliwahusisha wafanyakazi wa idara ya afya, taasisi zote za umma na za binafsi, wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri, waandishi wa habari na vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo.
“Wananchi wa mjini wana nafasi ya kupata elimu ya Ebola kupitia matangazo mbalimbali, lakini wananchi wa vijijini hawana nafasi hiyo, nashauri waelimishaji mwende vijijini, tumieni siku za soko wanapokuwa wamakusanyika; wafundisheni juu ya athari za ugonjwa huu hatari.” Alisema Lt. Col. Mntenjele.
Amesema kumekuwepo na mazoea ya kuwaelimisha viongozi; watendaji, madiwani na wenyeviti wa vijiji kwa matumaini kuwa watasambazi elimu waliyopata kwa wananchi, lakini uzoefu umeonyesha, wakishapata mafunzo hayo, hawayapeleki kwa wananchi.
Amewataka wataalamu kutoka mkoani na hata Wizarani watembelea maeneo ya vijijini, ambako kuna njia zisizo rasmi, zinazotumiwa na wananchi kutoka nchi jirani kuingia hapa nchini, kuliko kutembelea mipaka ya Rusumo na Kabanga.
“Kukitokea tatizo katika mojawapo ya nchi jirani hakuna mkimbizi au mhamiaji haramu atakayepita kwenye ‘scanner’ tulizoweka Rusumo na Kabanga; bali watatafuta njia iliyorahisi kwao kuingia nchini kwetu; hivyo, tujikite katika njia zisizo rasmi.” Alisema Lt. Col. Mntenjele.
Akitoa mfano, amesema wageni wanaopima ni wale wenye hati na kazi rasmi za kuja kufanya hapa nchini, lakini imedhihirika kuwa watu wa bodaboda wanapita tu bila kupima, huku akionya kuwa kwa mtindo huo wilaya ya Ngara iko katika hatari zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halamashauri ya Wilaya ya Ngara Ndugu Aidan Bahama, amezitaka kamati zilizoundwa kupambana na ugonjwa wa Ebola wilayani ngara, kuwajibika ipasavyo, ili kudhibiti ugonjwa huo, huku akionyesha wasiwasi wa kutokuwa na vitendea kazi vya kudhibiti ugonjwa huo.
“Nasikitika kwamba Wilayani kwetu hatuna vifaa vya kutosha kudhibiti ugonjwa huu; mbaya zaidi, vifaa vinavyotakiwa ni vya gharama kubwa, ambavyo Halmashauri yetu haina uwezo wa kuvinunua, kwani hata magari ya wagonjwa tuliyonayo; hayafai kuwasafirisha wagonjwa wa Ebola.” Alisema Ndugu Bahama.
Akatoa wito iandikwe barua ya kuomba vitendea kazi toka ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dr. Marco Mbata, ili vituo vya afya vilivyoko katika vijijiji vya mpakani, viweze kupata ‘toolkit’ mbili au tatu za kutibia wagonjwa wa Ebola kwa kila kituo ikiwa watapatikana.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngara Ndugu Vedastus Tibaijuka, ametoa angalizo kwa vyombo vya habari kutotoa taarifa za kusikia mtaani, badala yake wawasiliane na uongozi wa Wilaya ya Ngara, kwani kwa kufanya hivyo watatangaza habari za uhakika.
Amezitaka kamati kufanyakazi kama timu, kwani ugonjwa wa Ebola hauwahusu wafanyakazi wa afya tu, bali ni ugonjwa mtambuka unaozihusisha idara na vitengo vyote hapo wilayani; huku akionya kuachana na mila na desturi katika kupambana na ugonjwa huu, hasa katika suala la mazishi.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa