- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Wanafunzi 25 wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, wameacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito, na hakuna mhusika aliyekamatwa kwa kusababisha tatizo hili, ingawa kesi hizo zimeripotiwa kituo cha polisi.
Kaimu Afisaelimu Idara ya Sekondari wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara Ndugu James Marton, amekiambia kikao cha watendaji, wakuu wa shule za sekondari na msingi, na maafisaelimu kata wakati wa kikao kazi cha maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha I na wa darasa la I mwaka 2019.
“Kwa mwaka jana na mwaka huu takwimi tulizonazo jumla ya wanafunzi 25, wameacha shule, kwa sababu ya mimba; nawaomba watendaji wote, tulifanyie kazi kwa sababu hamna kesi yoyote, ambayo imeisha hukumiwa kati ya hizi.” Alisema Ndugu Marton.
Afisa huyo alisema tatizo hili ni kubwa, kwani idadi ya wanafunzi waliopotea kwa sababu ya mimba ni nusu ya darasa moja, huku akisema kwamba anatoa taarifa hiyo, ili watendaji pamoja na wakuu wa shule wajue hali halisi ilivyo.
Amezitaja shule zilizoathirika kwa tatizo la ujauzito zikiongozwa na kata ya kibimba, kuwa ni shule ya sekondari Rusumo ‘B’ wanafunzi 02, Shunga wanafunzi 03, Kanazi mwanafunzi 01, Mabawe mwanafunzi 02, Kibimba wanafunzi 04, na shule ya sekondari Murusangamba wanafunzi 03.
Shule nyingine ni Ndomba wanafunzi 02, Bukiriro wanafunzi 03, Rusumo wanafunzi 02, Ngara mwanafunzi 01, Muganza mwanafunzi 01, pamoja na Kirushya mwanafunzi 01 na kuongeza kwamba baadhi ya kesi hizi ziko polisi, wakati nyingine hazijulikani zilipo.
Baada ya taarifa hiyo, Afisa Tawala wa Wilaya ya Ngara Ndugu Vedastus Tibaijuka alisema suala la mimba katika shule za sekondari na msingi ni tatizo kubwa, kwani kuna wastani wa wanafunzi 10 kwa mwezi walipata ujauzito.
“Suala la mimba wastani wake kwa wilaya yetu ni mbaya, ukilinganisha na wilaya nyingine, tulipokaa kamati ya ulinzi na uslama ripoti kwa mwezi kwa wastani katika shule ya msingi na sekondari watoto wapatao 10, walipata ujauzito kwa mwezi; hili linatukwaza.”
Hili tatizo ni kubwa sana; wilaya nyingine watu wengependa kuwaheshimu wanafunzi, lakini kwa ngara wangependa kuoa, au kutembea na wanafunzi, kinachosikitisha zaidi wanaofanya vitendo hivyo ni watu wazima.
Amesema kesi zinaripotiwa polisi lakini zinapotea kwa sababu wazazi wanaficha ukweli na hawako tayari kutoa ushahidi; “kesi za mimba zikianza hivyohivyo, nyingi zinaishia kwenye vijiji na kata mtoto anapotea mzazi hayuko tayari kutoa ushirikiano.” Alisema Ndugu Tibaijuka.
Akitoa mfano, alikiambia kikao hicho kwamba anakumbuka wakati anasoma, mwalimu na Matroni walikuwa na uwezo wa kubaini watoto fulani Fulani, wenye wenye tabia mbaya wanawaonya kabla na matokeo yake yalikuwa mazuri sana.
Hata hivyo wasimamizi hao wa elimu, walisema tatizo la mimba linasababishwa na watoto kutembea umbali mrefu, huku wakidai kwamba wanafunzi hao wanapopanga vyumba, wazazi hawawahudumuii wala kuwatembelea, ili kujua mahitaji yao ya msingi.
Kwa maoni yao kujenga mabweni shuleni hasa kwa ajili ya watoto wa kike linaweza kuwa suluhisho la kudumu, kwani watoto hao watakuwa chini ya uangalizi wa walimu; huku wakiongeza kwamba pia itawasaidia kujifunza kwa umakini zaidi.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa