- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
“Nia ni kufanya biashara na uwekezaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara; kuwanufaisha wananchi kwa kulipa kodi kadiri mkataba unavyoelekeza, lakini pia tutasaidia katika sekta za maji, elimu, afya na barabara.” Alisema Mkurugenzi wa Mradi Ndugu William Mwingira.
Mkurugenzi wa Mradi Ndugu Mwingira alisema hayo Septemba 03, 2018 katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya, kwa niaba ya Kampuni ya FIIUP COMPANY LTD ya nchini Korea Kusini, kwamba awamu ya kwanza watawekeza katika kilimo cha kahawa na mpunga.
“Lakini siyo tu tutalima; tutanunua kahawa kutoka kwa wakulima, tutawapatia miche na elimu ya kuzalisha kahawa bora tukilenga kupata kahawa nyingi, kutoka kwa wananchi wanaotuzunguka; kwa hiyo tutainua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.” Alisema Mkurugenzi huyo wa Mradi Ndugu Mwingira
Amesema kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, watawahamasisha wananchi wote wanaozunguka mradi kwa kuwasambazia miche bora ya kahawa; huku akathibitisha kwamba kwa awamu ya kwanza mradi utatoa ajira za kudumu kwa watu 2500.
Aidha, wawekezaji hao watalipa kodi ya Halmashauri kama sheria ya kodi inavyoainisha, watalipa ‘service levy’ kadiri watakavyozalisha kwa mwaka; huku akidai kwamba mazao watakayozalisha hayatauzwa nchini, bali yatauzwa katika masoko ya nje ya nchi.
Ndugu Mwingira alisisitiza kwamba kwa sababu malengo yao ni soko la nje ya nchi wanataka kuwahamasisha wananchi wajihusisha katika kilimo cha kahawa na mazao mengine watakayoanzisha; huku akidai kwamba wamepata soko kubwa la avocados katika nchi za Ulaya Mashariki na Urusi.
Ameongeza kwamba wamepata soko la macadamia kwa hiyo wanataka kulianzisha wilayani Ngara; kwa hiyo wanatarajia kuomba eneo jingine la kuanzisha kilimo cha avocado na macadamia.
Aidha, kwa kuonyesha kwamba wana nia ya kufanyakazi pamoja na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, tayari wamekwisha andaa konteina la kompyuta, ‘photocopier machines’, ‘printers’ na vifaa vingine vya elimu ili watoto waweze kupata elimu nzuri.
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Lt. Col. Michael Mntenjele amesema serikali iko tayari kutoa ushirikiano, kwa kuhakikisha kwamba wawekezaji hao hawakwami katika shughuli zao, kwani lengo la wawekezaji ni kuwekeza fedha yao ili ilete matokeo chanya.
“Kwa hiyo tutatoa ushirikiano kwa kuhakikisha kwamba hawapati kikwazo chochote kwenye uwekezaji wao, na hatimaye malengo yao yaweze kufanikiwa.” Mkuu wa Wilaya ya Ngara Lt. Col. Michael Mntenjele aliahidi
Kampuni ya FRIIUP COMPANY LTD ni kubwa sana nchini Korea ya Kusini, inafanyakazi ya kusindika mazao ya vyakula kwa ajili ya wateja wake, walioenea katika nchi za Ulaya Mashariki, Urusi na Mashariki ya mbali.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa