- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
NGARA LEO
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Laurence Tax, tarehe 03 Mei, 2024 amezindua Kituo cha Afya Kilichopo Wilayani Ngara yalipo Makao Makuu ya Viteule K-9. Mhe Waziri Tax alishuhudia pia Makabidhiano kati ya Wizara na Kikosi cha Majengo ya kuishi Maafisa na Askari. Kwenye uzinduzi huo, Mhe Waziri Tax amesema kuwa Kituo hicho cha Afya ni muhimu na hatua ya kujivunia kwani kitatoa huduma za tiba kwa wanajeshi, familia za wanajeshi na wananchi wanaoishi maeneo jirani.
Akiongea na Maafisa na Askari pamoja na raia mara baada ya kukata utepe na kuashiria uzinduzi huo, Mhe Waziri Tax amemshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Aidha, amewapongeza viongozi, maafisa na maaskari waliosimamia na kushiriki katika ujenzi huo kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa vigezo na kuzingatia thamani ya fedha. Akasema "Dhamira ya Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma zinazohitajika" alisema Mhe Waziri Tax.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa amewashukuru pia Maafisa na Askari kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwa kujituma, weledi na uhodari katika utekelezaji wa majukumu yao na akasisitiza umuhimu wa kusimamia na kutunza majengo yaliyozinduliwa, vifaa tiba na visima vilivyokabidhiwa ili vidumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa muda mrefu.
Aidha, Waziri Mhe Stergomena Tax amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Ngara Mhe Col Mathias Julius Kahabi na Kamati ya Usalama ya Wilaya pamoja na taasisi zote za Serikali zilizoshiriki na kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo, na kuwataka kuendeleza ushirikiano ili kuimarisha ulinzi na huduma kwa ustawi wa wapiganaji na raia kwa ujumla.
Kabla ya kukata utepe wa kuzindua rasmi jengo la la Kituo cha Afya cha K-9 Waziri Tax alipata fursa ya kutembelea jengo hilo na kupata maelezo na kupanda mti wa kumbukumbu katika eneo la zahanati.
ngaradc.go.tz
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa