- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
“Msiwasajiri wahamiaji haramu katika taasisi zetu za elimu, bali muwaelekeze katika ofisi zetu za uhamiaji, ili tuwape vibali vya kusoma hapa nchi, tusipofanya hivyo tunaandaa mawaziri na viongozi wasio raia wa Tanzania.” Alisema Mkaguzi wa Uhamiaji Wilayani Ngara Ndugu Said Ali Malengo.
Ndugu Malengo ametoa rai hiyo, wakati wa Kikao cha Ushauri cha Wilaya, kilichofanyika Novemba 28, katika ukumbi wa Halmashauri chini ya uenyekiti wa mkuu wa Wilaya hiyo Lt. Col. Michael Mntenjele.
Tatizo la wahamiaji kusoma katika tasisi za elimu hapa nchini, linasababishwa na viongozi katika mashina wasiokuwa wazalendo, kwa sababu wanapotaka kwenda shule wanapewa barua ya kupata cheti cha kuzaliwa na viongozi hao.
Wahamiaji haramu si raia wa Tanzania wanaposoma katika taasisi za elimu hapa nchini wanatumia gharama kubwa za taifa, ambazo kihalali si haki yao na haziwahusu, hivyo wanazikosa watanzania, ambao kimsingi ndio wenye haki nazo.
Mme aliyemuoa mke mhamiaji anatakiwa kuripoti ofisi ya uhamiaji, ili apate kibali cha ukaazi ambacho atakilipia shilingi 100,000 au dola 50, na akiwa na watoto watakapofikia umri wa kwenda shule atapewa kibali bure cha kuwaruhusu watoto hao kusoma hapa nchini.
Lengo la kumpatia kibali hicho, ni kumkumbusha kwamba yeye si mtanzania ni mhamiaji, kwa hiyo, hata akisoma kwa kiwango gani tayari, atakuwa na rekodi inayomuonesha kwamba yeye si raia wa Tanzania, bali ni mhamiaji.
Amekikumbusha kikao hicho, kwamba raia wa kigeni anapoingia hapa nchini, lazima awe na viza na ikiwa ni mwanachama wa nchi za Afrika Mashariki, atapata visa ya matembezi aliyoiita ‘Holyday visa’ bila malipo yoyote.
Mhamiaji anapokuwa na visa ya matembezi haruhusiwi kuhusika kwa namna yoyote ile katika shughuli ya kiuchumi, na ikiwa mwenyeji wake, anataka kumtumia itabidi aende ofisi ya uhamiaji, amlipie dola 100 itayodumu kwa muda wa miezi mitatu, kinyume chake atalipa faini ya dola 600 au kifungo.
Aidha, amesema ili kuepuka hilo, wanapokamata wahamiaji haramu wanakamata aliyehamia na aliyemleta hapa nchini; “sisi na polisi ni wamoja tunapofanya operation tunawakamati wahamiaji na wamiliki wa wahamiaji hao.” Alisema Ndugu Malengo.
Kwa sababu wakiachwa wamiliki wa wahamiaji haramu, matokeo yake wamiliki wa wahamiaji hao, wanawakaribisha tena; kwa hiyo, dawa ni kuwakamata wote; wahamiaji na wamiliki wao.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa