- Mwanzo
- Kuhusu sisi
- Utawala
- Fursa za uwekezaji
- Huduma zetu
- Madiwani
- Miradi
- Machapisho
- Kituo cha Habari
Wakuu wa shule za sekondari, Maafisaelimu Kata, Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, wametakiwa kuchukua hatua za kudhibiti utoro shuleni, kulikopelekea wanafunzi wapatao 673 kutoroka katika kipindi cha 2017 na 2018.
Hayo ni kwa mujibu wa Kaimu Afisaelimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara Ndugu Marton James, wakati wa kikao kazi cha maadalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidoto cha kwanza na wa darasa la kwanza 2019, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri Desemba 05, 2018.
“Kuna utoro uliokithiri katika shule zetu za sekondari watoto wengi wanapotea, na mnajua serikali inatoa gharama kubwa, kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi hawa; katika mwaka 2017 na 2018 tumepoteza jumla ya wanafunzi 637.” Alisema Ndugu Marton.
Amefafanua kwamba kati ya wanafunzi hao; wavulana waliotoroka ni 340, ambapo wasichana wapatao 297 wametokomea, huku akizitaja shule zinazoongoza kwa utoro kuwa ni shule ya sekondari Bukiriro iliyopoteza wanafunzi 112.
Shule nyingine zinazoongoza kwa utoro ni shunga na Nyakisasa sekondari, lakini hakutaja idadi ya wanafunzi watoro; huku akiwataja wanafunzi wa shule ya Kibogora kuwa ni 58, Rusumo imepoteza wanafunzi 52, Ngara sekondari wanafunzi 57, na Muyenzi imepoteza wanafunzi wapatao 33.
Amewapongeza wakuu wa shule za sekondari za Ntobeye, Nyabisindu, na Lukole kwa kudhibiti utoro, kwa madai kwamba vyanzo vyao vya taarifa vinaoonyesha shule hizo ndizo pekee, ambazo wanafunzi hawatoroki shuleni.
Aidha, amefafanua kwamba wanafunzi aliowataja kuwa watoro, wameacha kusoma kwa muda wa siku tisini, yaani miezi mitatu mfululizo bila kuhudhuria shuleni; “utoro ninaozungumzia mwanafunzi, akishakaa nyumbani zaidi ya siku 90, huyo siyo mwanafunzi tena.” Alisema Ndugu Marton.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Kibogora Mwalimu Aquiline Gwimo, akichangia hoja alisema moja ya sababu za utoro, wanafunzi kutembea mwendo mrefu, kutoka shuleni hadi nyumbani, kwani umbali huo unawachosha wanafunzi, wengine wanakata tamaa na kuamua kuacha shule.
Ameshauri kuwepo mpango wa kujenga mabweni, kwani hayo yatawasaidia wanafunzi kusoma kwa utulivu, huku walimu wakiwa na nafasi nzuri ya kuwadhibiti wakati wote wanapokuwa shuleni.
Aidha, wazazi wametuhumiwa kwa kuchangia katika tatizo hili, kwa madai kwamba hawawafuatilii watoto wanaporejea nyumbani wakati ambao si wa likizo, ili wajilidhishe ni kwa nini mtoto hayupo shuleni.
Naye Afisa Tawala wa Wilaya ya Ngara Ndugu Vedastus Tibaijuka, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo, na kuwataka maafisaelimu kata na wakuu wa shule za sekondari, kuliona tatizo hili na kulichukulia kwa uzito unaostahili na kulidhibiti.
“Mambo haya yanasikitisha sana, jamii yetu ya ngara, wazazi wanapenda watoto wafanyekazi za ndani, mtoto anakuwa darasa la tano au la sita, mzazi ameisha muadalia mazingira ya kwenda kufanyakazi ndani Kahama au sehemu nyingine.” Alisema Afisa Tawala Tibaijuka.
Ameitaka jamii ibadilika na ione umuhimu wa elimu kwa watoto wao, huku akisistiza kwamba Ngara haiwezi kuendelea kuwa duka la watoto wa kufanyakazi za ndani, bali iwe kitovu cha watoto wasomi.
Ngara District Council
Anuani ya Posta: P.O.Box 30, Ngara
Simu ya mezani: 0282226016
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@ngaradc.go.tz
Hakimilki ©2017 Halmashauri ya wilaya ya Ngara. Haki zote zimehifadhiwa